Aishi Manula! Ni miongoni mwa wanadamu wanaoishi hewani kwa sasa. Anaelea kama puto. Mara zote puto huwa linaelekea hewani bila ya mwelekeo. Ndivyo anavyoishi Manula kwa sasa. Watu hawajui yuko wapi na anafanya nini.
Majuzi tumesikia ameanza mazoezi kwa mara nyingine tena katika timu yake ya Simba. Hakutambulishwa kama mchezaji wa Simba siku ya 'Simba Day’ na kabla ya hapo hakuwa katika kundi la wachezaji wa Simba waliokwenda kupimwa afya kabla ya maandalizi ya msimu mpya.
Kabla ya hapo pia hakuwa katika kundi la wachezaji wa Simba waliokwenda Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya ulioanza wikiendi hii duniani kote. Katika lugha ambayo wengine tunaielewa ni, Aishi hatakiwi Simba.
Ametajwa ni mmoja wa wachezaji ambao wameihujumu Simba katika miaka ya karibuni. Kwamba amehusika kuwafanya watani wawe kileleni kwa miaka hii ya karibuni ambayo wamekuwa wakitembea kifua wazi ndani na nje ya Tanzania.
Katika maneno mengi ya mitaani ni, hata Aishi mwenye haitaki Simba. Amechoshwa na shutuma nyingi dhidi yake. Hata hivyo, kuna mdudu ambaye yupo kati ya Aishi na Simba. Inadaiwa Simba haitaki kumuachia Aishi kirahisi.
Vyovyote ilivyo, katika mtazamo huru zaidi ukweli ni kwamba Aishi lazima acheze soka. Kwa gharama yoyote ile, Aishi lazima acheze soka. Iwe katika lango la Simba au kwingineko, Aishi lazima acheze soka. Amejikuta katika nyakati ambazo taifa lazima liingilie kati katika ugomvi wake na Simba.
Ama akae langoni na kugombania nafasi yake na kipa mpya wa Simba, Moussa Camara au aende kwingineko na kuwa kipa wa kwanza. Taifa linamhitaji Aishi. Kuna sababu lukuki la kuwa katika hali hii. sababu ya kwanza na ya msingi ni ukweli, katika miaka ya karibuni yeye ndiye ambaye amekuwa ‘Tanzania One’.
Unawatazama makipa wengine nchini kisha unagundua ukweli hakuna kipa kama yeye. Licha ya kwamba ana kipaji lakini amejikusanyia uzoefu mwingi wa mechi za kimataifa kupitia klabu yake ya Simba na kisha timu ya taifa.
Aishi anawaacha mbali makipa wengine katika suala hili. Hapo hapo unajaribu kuwaza na kugundua katika miaka ya karibuni katika hizi timu zetu kubwa Aishi ndiye kipa ambaye alikuwa anatubeba. Nafasi nyingine zote zimekwenda kwa makipa wa kigeni.
Tazama katika ‘Top Four’ ya msimu uliopita Aishi ndiye kipa ambaye angejitokeza katika orodha ya makipa wa kizawa kama angekuwa anakaa langoni. Tuna Yanga, Azam, Simba na Coastal Union. Aishi ndiye kipa pekee mzawa ambaye angeweza kuchuana na makipa wengine katika nafasi hii.
Katika kila hali Aishi analazimika kurudi langoni kwa sababu hatuna jinsi. Kama ingekuwa zamani suala la Aishi lingekuwa dogo lakini kwa kadri siku zinavyosonga mbele na namna ambavyo vipaji vinapotea katika soka tunalazimika kulazimisha kuona Aishi anacheza soka katika Ligi kuu akiwa katika klabu yoyote ile.
Zamani usingekuwa na wasiwasi kwa sababu tulikuwa na makipa wengi. Miaka hiyo ya 1970 tulikuwa na kina Juma Pondamali, Athuman Mambosasa, Omar Mahadhi na wengineo. Halafu tukasogea zama za kina Idd Pazi, Hamis Kinye, Ramadhan Korosheni, Joseph Fungo na wengineo.
Baadaye tukaja zama za kina Ally Bushir, Riffat Said, Mohamed Mwameja, Joseph Katuba, Madatta Lubigisa na wengineo. Maisha yalitufanya tupumzike. Makipa walipungua zaidi tukafika zama za Juma Kaseja na Ivo Mapunda. Mwishowe kabisa tukabakia na Manula. Huyu alibakia kuwa ‘Tanzania One’ huku akiwa amewaacha mbali wenzake tofauti na zamani viwango vya makipa vilikuwa havitofautiani.
Lakini sasa amezungukwa na siasa nyingi za mpira wetu. Hatujui kama Aishi yupo sahihi au wanaomshutumu katika mambo mbalimbali wapo sahihi. Kitu ambacho tunafahamu ni Aishi lazima acheze soka kwa sasa kwa sababu ya masilahi ya taifa.
Kama tungekuwa na makipa wengi wazuri kwa pamoja kama ilivyokuwa zamani basi wala tusingejali sana kuhusu yeye. Lakini kwa hali ilivyo sasa kuna umuhimu wa kujali. Yeye ndiye kipa namba moja kwa taifa na unapokuwa mchezaji kitu cha msingi ambacho kinapaswa kulinda kipaji chako ni kucheza mara kwa mara.
Aishi kukaa nje hakulisaidii taifa. kuna mchuano mkubwa katika nafasi za ndani lakini sio katika nafasi ya langoni. Aishi anahitaji kucheza soka. Anahitaji kuwa langoni. Anahitaji kucheza. Hili sio jambo la masilahi yake binafsi bali ni kwa masilahi ya taifa.
Wakati mwingine taifa linapaswa kuingilia kati mambo kama haya kwa masilahi ya taifa. kuna wakati Wabrazil walimwambia Neymar lazima aende akacheze soka la kulipwa Ulaya ili awe na uzoefu wa kutosha kuelekea kombe la dunia la mwaka 2014 ambalo lingefanyika nchini kwao Brazil mwaka 2014.
Ndiyo maana Neymar aliondoka Brazil kwenda kucheza Barcelona mwaka 2013. Hii ni kama ilivyo kwa Aishi kwa sasa. Tunakabiliwa na michuano ya kufuzu kwenda Afcon mwaka 2025. Tunakabiliwa na michuano ya Afcon 2027 ambayo sisi tutakuwa wenyeji. Aishi anapaswa kuwa langoni.
Haijalishi kama Simba ipo sahihi au Aishi yupo sahihi lakini Aishi anaihitajika langoni haraka iwezekanavyo. Yeye mwenyewe anaweza kujitafakari vizuri zaidi lakini katika upande wa sisi ambao tunalitazama zaidi taifa kuliko siasa za vilabu vyetu nadhani ni jambo jema Aishi akiwa langoni hata kama atakuwa katika lango la Pamba FC ya pale Mwanza.
Edo Kumwembe
from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/AwkvV0c
via IFTTT