Jeshi la Polisi nchini limepiga marufuku magari binafsi kutumika kusafirisha abiria kwa maelezo kuwa mbali na kuwa ni kinyume cha sheria, lakini pia ni hatari kwa usalama wa abiria na madereva.
Akizungumza mjini Musoma leo Jumapili Septemba 22, 2024, wakati wa ukaguzi wa magari ya abiria, Mkuu wa Takwimu za Makosa ya Barabarani kutoka Kitengo cha Trafiki Makao Makuu, Mwashamba Onesmo amesema wamiliki na madereva wa magari binafsi wanapaswa kutenga bajeti ya kutosha wanapopanga kusafiri badala ya kutegemea nauli za abiria wasiokuwa rasmi.
“Pamoja na kuvunja sheria za usalama barabarani, pia wote mnakuwa hatarini, mfano dereva umepakia abiria ambao hauwafahamu unaweza kufika huko mbele wakakugeuzia kibao au wewe abiria umepanda kwenye gari lisilokuwa rasmi unafika mbele, dereva anakugeuzia kibao mwisho wa siku madhara yanatokea, mfano kutekwa, kuuwawa na kuibiwa,” amesema.
Pia, amewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kwamba kuanzia sasa madereva watakuwa wakitozwa faini kwa kila kosa wanalofanya wanapokuwa safarini.
“Kuna ile tabia eti ukitozwa faini mara moja kwa siku ukalipia, sasa unakuwa kama umeruhusiwa kufanya makosa mengine barabarani kwa siku hiyo, eti ukikamatwa unasema tayari umelipa faini.”
“Kuanzia sasa utakuwa unatozwa faini kwa kila kosa, hatutajali tayari umelipia kosa lingine, kosa la eneo moja halizuii kutozwa faini kwa la eneo jingine hata kama ikitulazimu kukuandikia faini mara tano kwa siku katika maeneo tofauti tutafanya hivyo,” amesema.
Amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kubaini baadhi ya madereva kuwa na tabia ya kutenga pesa kwa ajili ya faini ya kwanza ambapo wakishalipa wanavunja sheria za usalama barabarani makusudi, ikiwamo kuendesha mwendokasi na kuhatarisha usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara wakijua hawatawajibishwa.
Akizungumza kuhusu magari binafsi kutumika kusafirisha abiria, Kamanda wa Trafiki Mkoa wa Mara, Matthew Ntakije amesema kuanzia sasa wanaanza msako wa kuwakamata madereva wa magari hayo pamoja na wapiga debe wanaotafuta abiria kwa ajili ya magari binafsi.
“Ukiwabeba hawa watu, mkisimamishwa na trafiki unasema hao ni ndugu zako lakini kiuhalisia mnakuwa hamfahamiani na mkipata shida huko mbele, lawama zinakuwa kwetu, hii tabia tunatakiwa kwa pamoja tuikomeshe,” amesema Ntakije.
Baadhi ya mawakala wa mabasi katika stendi kuu ya Musoma wamesema tabia ya magari binafsi kubeba abiria imekuwa ikichangia wao kupata hasara, hivyo ni vema mamlaka husika zikazuia hali hiyo.
“Mimi nalipia ushuru, tozo na kodi nyingine wakati huohuo hapa stendi magari yanaondoka kwa muda maalumu sasa gari linashindwa kujaza kwa sababu abiria hawaingii ndani badala yake wanapanda magari binafsi nje ya stendi, ukumbuke hao wenye magari binafsi hawalipii chochote,” amesema Tizo Mustafa.
Selemani Wambura amesema ni vema kwa yeyote anayetaka kusafirisha abiria akafuata taratibu ikiwa ni pamoja na kusajili magari yao kwa ajili ya shughuli hiyo, ili waweze kufuata utaratibu wa stendi ambao ni kupanga foleni ili abiria waingie stendi, jambo ambalo pia litawasaidia kufanya shughuli zao kwa tija.
Baadhi ya abiria wamesema utaratibu wa ukaguzi wa magari ya abiria unatakiwa kuwepo kila siku ili kuepuka ajali zisizokuwa za lazima
“Mfano askari anaingia kwenye gari anawaambia abiria wafunge mikanda wakati gari halina mikanda, kwa hiyo napendekeza wawe na utaratibu wa kukagua magari mapema ili gari lenye mapungufu lisiruhusiwe kuwepo kwenye foleni ya kupakia hadi lirekebishwe,” amesema Anna Kuboja.
from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/RE2O4Q6
via IFTTT