Mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva, 30, ameeleza mikakati yake wakati akitua Jamhuri ya Iraq huko Asia Magharibi kwa ajili ya kujiunga timu yake mpya, Al Talaba SC iliyomsajili kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Msuva ambaye alikuwa nchini kwa zaidi ya miezi mitatu tangu kumalizika kwa msimu uliopita ambao alikuwa akiichezea Al-Najma ya Saudi Arabia, amesema hii ni fursa nyingine tena kwake kuendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania nje ya nchi.
“Nina uzoefu wa kutosha kwa hiyo nahitaji kuendeleza kile ambacho nimekuwa nikikifanya kwa miaka mingi, Al Talaba SC walinitafuta baada ya mkataba wangu kumalizika kule Saudia na nikawaeleza mahitaji yangu na kwa bahati nzuri walikuwa tayari kunipa nilichohitaji,” anasema na kuongeza;
“Kilichobaki kwa sasa ni mimi tu kuwafanyia kazi yao, binafsi sina shaka na uwezo wangu nipo tayari kuonyesha Tanzania ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yenye vipaji vingi vya soka. Ninashauku kubwa ya kuanza maisha yangu mapya ya utafutaji Iraq, najua ni nchi nzuri kama ilivyo Saudia.”
Kulingana na programu za mazoezi ambazo alikuwa akitumiwa, Msuva anaamini zitamsaidia kuwa katika mstari mmoja na wachezaji wengine wa timu hiyo.
“Mbali na ratiba ya timu, nilikuwa nikijituma mwenyewe kila siku ili niwe bora zaidi na hilo limekuwa likinisaidia. Binafsi nimejiandaa kutumika katika nafasi yoyote ambayo benchi la ufundi itapenda kunitumia.”
Al Talaba SC itakuwa timu ya sita, Msuva kuichezea nje ya Tanzania, timu lake la kwanza lilikuwa Difaa El Jadida alilojiunga nayo Julai 2017, baada ya kuonyesha makali yake ndani ya miaka mitatu kwenye ligi ya Morocco, Wydad Casablanca ilivutiwa naye na kumsajili lakini hakudumu kwa vigogo hao kutokana na ishu za madai zilizowafanya kufikishana Fifa.
Baadaye Msuva aliibukia Saudi Arabia ambako alianza kwa kuichezea, Al-Qadsiah mkataba wake ulipomalizika alirejea Afrika kwa kujiunga na JS Kabylie ya Algeria lakini mambo hayakumwendea vizuri mkataba wake ulikatishwa na ndipo alipoamua kurejea tena Saudia kwa kujiunga Al-Najma aliyoichezea msimu uliopita.
LIGI YA MABINGWA
Msuva ana ndoto ya kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Asia ambayo timu ya Cristiano Ronaldo, Al Nassr ya Saudi Arabia ilishiriki na kuishia hatua ya robo fainali ambapo waliondolewa na Al Ain ya Falme za Kiarabu.
Jambo la kwanza natakiwa kwenda kupambana na wachezaji wenzangu ili tutwae ubingwa kwa kufanya hivyo tutakuwa tumejiweka katika nafasi ya kucheza michuano ya ligi ya mabingwa, itakuwa ni nafasi nyingine nzuri kwangu,”
“Nimecheza ligi ya mabingwa Afrika na kufanya vizuri hivyo nahitaji kucheza michuano ya namna hiyo Asia, najua kwamba haitakuwa kazi nyepesi kwa sababu mpira wa Iraq unaushindani mkubwa kama ilivyo kwa Saudia,” anasema.
Msimu uliopita Al Talaba SC ilishika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi yenye timu 20 hivyo wanakibarua kizito mbele yao kuhakikisha wanaivua ubingwa Al Shorta.
MWELEKEO WAKE
Licha ya kuwa na miaka 30, Msuva anajiona bado ana nafasi ya kuendelea kucheza soka la kulipwa nje ya nchi; “Najiona kuwa na miaka mingine minne hadi mitano ya kuendelea kucheza soka mbali na nyumbani japo siwezi kusema kwamba nitarudi Tanzania kumalizia mpira wangu wakati gani,”
“Hili nimekuwa nikiliweka wazi kila wakati, nahitaji kumalizia mpira wangu nyumbani Tanzania, baada ya hapo ndio tutaona nini kinaweza kufuata.”
NAFASI YA STARS
Msuva anaiona Tanzania ikiwa bado na nafasi ya kufuzu kwa fainali za Afcon 2025 pamoja na kuanza kwa sare ikiwa nyumbani dhidi ya Ethiopia.
Sitaki kuamini kwamba eti kwa sababu fulani hakuwepo ndio maana tumeanza kwa suluhu, ile timu ya taifa na sio ya mtu fulani kila ambaye anapata nafasi anawajibu wa kupambana kwa ajili ya nchi, tukikwama tumekwama wote na sio kuanza kumnyooshea vidole fulani,” anasema na kuongeza;
“Walimu watakuwa wameona wapi ambapo ilikuwa changamoto kwetu katika mchezo wa kwanza kiasi cha kushindwa kupata matokeo ya ushindi na watarekebisha kwenye uwanja wa mazoezi ili tufanye vizuri kwenye mchezo unaofuata, kiukweli tuna timu nzuri ambayo inaweza kupambana, tunatakiwa kuiunga mkono.”
Kuhusu nafasi yake Stars, Msuva anaamini bado ipo lakini kutokana na kuwa kwake nje ya uwanja kwa muda mrefu ndio maana hakuwa sehemu ya kikosi hicho; “Niliongea na kocha na kumweleza nini kinaendelea kwa upande wangu kabla hajaita kikosi cha Stars, na tuliukuwa na makubaliano rasmi, naamini baadaye nitarudi tena Stars.”
MZIZE MTU
Miongoni mwa wachezaji ambao wanamvutia Msuva kwa sasa ni pamoja na mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize ambaye kwa sasa amekuwa akihusishwa na klabu mbalimbali kubwa barani Afrika ikiwemo Wydad Casablanca.
“Kuna wachezaji wengi ambao kwa sasa wanakuja vizuri, Mzize ni mmoja wapo, namwona akiwa na nafasi kubwa ya kuendelea kufanya vizuri,” alisema Msuva.
from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/ypq06kN
via IFTTT