Mzize Ajipata Afunguka Haya 'Mimi ni Hatari Zaidi Nikianzia Benchi'

 

Mzize Ajipata Afunguka Haya 'Mimi ni Hatari Zaidi Nikianzia Benchi'

Straika wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, Clement Mzize, amesema yeye ni hatari zaidi akitokea benchi kuliko akianza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo inayofundishwa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi.


Mzize ambaye yuko katika rada za Wydad Casablanca ya Morocco na timu nyingine mbalimbali, aliliambia Nipashe ana kipaji cha kuusoma mchezo na makosa ya wapinzani kabla ya kwenda kuyafanyia kazi na ndio sababu amekuwa akifanya vizuri anapotokea benchi.


Alisema amekuwa na uwezo mzuri wa kwenda kurekebisha makosa ya wenzake na kuongeza nguvu pale panapohitajika na sababu hiyo anafurahia zaidi kuanzia benchi badala ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza. 


"Kama mnavyoona mimi nikiingia kipindi cha pili ninakuwa moto kwa sababu kuna kitu nakuwa nimekisoma, walinzi wa timu pinzani wana makosa fulani wanayafanya, nikiingia nakufanyia kazi na nyinyi wenyewe mnaona huwa kinatoa majibu mazuri," alisema Mzize.


Aliongeza si kwamba yeye anaomba awekwe benchi ili aingie kipindi cha pili na kufanya hivyo, bali ni mipango ya Gamondi, ambaye huenda tayari ameshaona akiingia anampa matokeo chanya katika kikosi chake.


"Kutokea benchi ni mipango wa mwalimu, anaweza kukupa mechi moja uanze, nyingine ukae nje kwanza, ila mimi namshukuru Mungu, maana unaweza kuanzia nje na usifanye vizuri na ukaanza pia usifanye kile kinachotakiwa.


Ila niseme tu ukiwa nje na wenzako wanacheza ndani kwangu mimi nakuwa na uwezo wa kuusoma mchezo vizuri, udhaifu wa wapinzani na safu ya ulinzi, unaona ukikaa pale, ukifanya hivi, basi utafanya kitu tofauti na kuisaidia timu," Mzize aliongeza.


Nyota huyo alisema pia ingawa mguu wake wa asili anaotegemea katika soka ni wa kulia, lakini mguu wa kushoto ndiyo ina nguvu zaidi ya kupiga mashuti, kukokota mpira na kutoa pasi kuliko wa kulia.


"Mimi mguu wangu ni wa kulia, lakini mguu wa kushoto unakuwa na nguvu zaidi kwa kutoa pasi na kukokota mpira na uko vizuri kufanya hivyo kuliko wa kulia na hiki kitu hakikuja kwa bahati mbaya, nimejifunza na nimefanya hivyo kwa kuwaangalia wachezaji wa nje akiwamo Cristiano Ronaldo, yule jamaa mguu wake wa kulia, lakini akipiga kushoto kama kulia.


Kwa sasa akitaka kuwa mchezaji bora ni lazima uwe una uwezo wa kutumia mguu yote miwili, hata kama haitokuwa na nguvu sawa, lakini ikaribiane," aliongeza mchezaji huyo.


Katika msimu mpya ulioanza, Mzize amecheza mechi sita, mbili akianza na nne akitokea benchi ambapo mara nyingi  anafunga na kuwa hatari kwa mabeki, amesema huwa hakai benchi tu na kuangalia soka, bali anakuwa na kazi ya  kocha ya kuusoma mchezo, kujua timu pinzani ina mapungufu wapi, hasa eneo ya mabeki.


Timu nyingine ambazo zimeonyesha nia ya kutaka huduma ya Mzize ni Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Aalborg BK ya Denmark na Crawley Town FC inayocheza Ligi Daraja la Pili nchini Uingereza.


Mchezaji huyo alifunga bao la pili katika mechi ya kwanza ya msimu ya Yanga iliyomaliza kwa ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Kagera Sugar, goli la kwanza likipachikwa na Mkongomani Maxi Nzengeli.


Yanga pia imesonga mbele katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuiondoa Vital'O ya Burundi kwa kuwafunga mabao 10-0 na sasa hatua inayofuata itakutana na mabingwa wa Ligi Kuu Ethiopia, CBE.



from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/O8H15dK
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post