WATU 14 wamefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari matatu, likiwamo lori na costa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana katika eneo la Kikavu, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.
Alisema lori aina ya FAW lenye namba T 517 EAE na tela namba T 287 CYF liligonga kwa nyuma gari T 553 aina ya Toyota Hilux na kisha kupoteza mwelekeo na kwenda kugongana uso kwa uso na gari aina ya Costa T 525 DKP.
Babu ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, alisema wakati huo, Toyota Coaster ilikuwa ikitokea Moshi mjini kwenda Arusha.
Alisema katika ajali hiyo, watu sita walifariki dunia papo hapo na wengine wanane walifariki dunia njiani wakipelekwa hospitalini.
Kwa mujibu wa Babu, majeruhi wa ajali hiyo wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Hai, Hospitali ya Rufani ya Kanda ya KCMC na Hospitali ya Rufani ya Mkoa Mawenzi.
“Tunasikitika sana kupoteza nguvu kazi ya watu 14 ambao walikuwa wanakwenda katika shughuli zao na nitumie nafasi hii kutoa pole kwa ndugu wote waliopoteza wapendwa wao, lakini tuzidi kuwaombea majeruhi wote wapone haraka na kuendelea na shughuli zao,” alisema Babu.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi, ili kubaini chanzo cha ajali hiyo, huku akitoa wito kwa madereva kuwa makini wanapoendesha vyombo vya vya moto hasa nyakati za usiku.
“Kama mnavyotambua barabara zetu ni nyembamba sana, maeneo haya yanaruhusu gari moja kupita na sio kupishana hivyo, niwaombe chukueni tahadhari sana mnapokuwa barabarani,” aliagiza Babu.
Baadhi ya majeruhi akiwamo, Tunu Hassan, ambaye amelazwa hospitali ya Mawenzi, aliiomba serikali kuendelea kudhibiti madereva walevi, ili kupunguza ajali zinazozuilika.
"Sijui nini kimetokea ila niliona gari linakuja mbele yetu na ghafla nimejikuta hospitalini. Niiombe serikali ifanye jambo hasa katika upanuzi wa barabara katika eneo la Kikavu,” alisema majeruhi mwingine, Happy Ngowi.
Msemaji wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa Mawenzi, Vena Karia, alisema wamepokea majeruhi 11 huku wawili kati yao wakiwa watoto, nane ni watu wazima na watano wamehamishiwa KCMC, kwa matibabu zaidi kutokana na hali yao.
from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/JDtlWa3
via IFTTT