BAADA ya timu zao kupata ushindi kwenye michezo ya juzi, makocha wa Azam FC, Rachid Taoussi na wa Singida Black Stars, Patrick Aussems, wamesema msimu huu wanautaka ubingwa wa Tanzania Bara ambao kwa misimu 11 imekuwa ikihodhiwa na klabu za Simba na Yanga.
Wakizungumza mara baada ya mechi zao zilizochezwa Dar es Salaam na Singida, makocha hao wamesifu ushindani mkubwa uliopo msimu huu, wakisema itabidi timu za Simba na Yanga zifanye kazi ya ziada kama zinautaka ubingwa.
Juzi mchana kwenye Uwanja wa Liti Singida, Singida Black Stars ilimaliza dakika 90 na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate, mabao yakiwekwa wavuni na Josephat Banda dakika ya 54 na Ayoub Lyanga, dakika ya 65, ambayo yamezidi kuiweka timu hiyo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikifikisha pointi 22, ikiwa imecheza michezo minane, ikishinda saba na kutoa sare mmoja.
Usiku, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Azam iliishindilia KenGold mabao 4-1 mabao yaliyowekwa kwenye kamba na Feisal Salum, Jhonier Blanco, Gibril Sillah na Cheikh Sindibe, huku la KenGold likifungwa na Joshua Ibrahim.
Ni matokeo yameifanya Azam kushika nafasi ya nne ikifikisha pointi 18, ikicheza michezo tisa na kuzidi kuweka shinikizo kwa timu za juu ya msimamo.
"Tuna furaha kwa ushindi kwa sababu tunazidi kupaa juu ya msimamo, nimekitengeneza kikosi na naona kimeanza kunipa kile ambacho nilikuwa nahitaji.
Nataka timu yangu icheze mpira wa kasi, wachezaji wangu wasikae na mpira sana, mara moja wameuachia, lakini pia wajitoe na kupambana, tukifanya hivi tunaweza kutwaa ubingwa ambao upo wazi, yoyote anaweza kuchukua, hata sisi msimu huu kwa kikosi hiki tunaweza kuupata," alisema Taoussi.
Naye Aussems amesema ushindi wanaopata ni kielelezo tosha kuwa wanataka kufanya mabadiliko kwenye nafasi ya juu msimu huu.
"Tumeongoza ligi kwa kipindi kirefu, nia yetu ni kukaa pale mpaka mwisho ingawa si rahisi, lakini tunataka kule juu kuwe na mabadiliko," alisema.
from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/uq7YbNF
via IFTTT