KIBU DENIS ASIPOKAA VIZURI MPANZU ANAKUJA KUMWARIBIA SIMBA
Kibu Denis 'Mkandaji' bado hajarudi katika kile kiwango alichokuwa nacho alipotua kwa mara ya kwanza Msimbazi msimu wa 2021-2022 alipofunga mabao manane, sasa wakati akiendelea kujitafua vyema kikosini mara paap! Mabosi wa klabu hiyo wamemshusha winga mwingine mkali kutoka DR Congo, Elie Mpanzu.
Jambo hilo la kusajiliwa kwa Mpanzu ambaye kwa sasa anasikilizia tu, kujua anachukua nafasi ya nani kabla ya kuanza kuwasha moto kikosini, limemfanya Kibu ashtuke na fasta kutoa msimamo wa kuipigania namba mbele ya Mkongoman huyo na mawinga wengine wa kikosi hicho cha kocha Fadlu Davids.
Kibu amefichua kuwa ujio wa Mpanzu kwa sasa unageuka kuwa chachu ya kuamsha morali wa kujituma zaidi akiwa na kikosi hicho ili kuhakikisha anaendelea kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza cha kocha Fadlu.
Kibu alitoa msimamo huo, alipouliwa na Mwanaspoti juu ya kutua kwa winga huyo Mkongoman kutampa changamoto gani, ikizingatiwa kuna mawinga wengine wanaomfanya wakati mwingine kuanzia benchi naye alijibu kwa kusema; "Napenda ushindani, utafanya niongezee bidii ya mazoezi, ili kumshawishi kocha kuendelea kuniamini kunipa nafasi ya kucheza."
Kibu aliyetua Msimbazi misimu mitatu iliyopita akitokea Mbeya City aliofafanua kuwa; "Hata ningeletewa Cristiano Ronaldo wa Al Nassr, bado ningefurahia kucheza naye, kwani ubora wake ungenifanya niwe bora zaidi, hivyo sijawahi kukata tamaa, wala kuogopa kupambania namba, maisha hayataki mtu anayekata tamaa, bali yanahitaji kujituma na kuiamini kesho ni bora zaidi ya jana."
Kibu ambaye msimu uliopita, alifunga bao moja katika Ligi Kuu, alisema nje na Mpanzu ndani ya kikosi hicho kina ushindani kila eneo ni juu ya mchezaji mwenyewe kujituma na kumpa urahisi kocha Fadlu, kujua nani amtumie muda gani na mechi gani.
"Mtazamo unaweza ukafanya mchezaji afanye vizuri, ama afeli ndio maana nasisitiza napenda ushindani, unasnifanya nijitume kwa bidii, kuliko kujibweteka na kuona nimemaliza kazi," alisema Kibu aliyefunga moja ya mabao yaliyoing'oa Al Ahli Tripoli ya Libya kwa mabao 3-1 katika mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kibu alifichua kuwa, licha ya kucheza kama mshambuliaji, lakini ana uwezo wa kumudu kukipiga eneo la ulinzi kama beki na mambo yawa freshi tu.
"Nina uwezo wa kucheza kama beki wa kulia, ndivyo ilivyo kwenye soka la kisasa na winga yoyote anaweza akafanya jukumu hilo, ndio maana unaona naweza kushambulia na kuisaidia timu kukaba," alisema Kibu, huku kocha Fadlu alimzungumzia mchezaji huyo kwa kusema; "Ni mchezaji mzuri, napenda anavyoshambulia na kuisaidia timu kukaba, ila wachezaji wote wanahitaji muda ili kuwa sawa, ndio kwanza ligi imeanza, naamini tutafanya vizuri."
from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/gshrL8q
via IFTTT