MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, pamoja na wafuasi 11 waliokuwa wanashikiliwa na polisi, wameachiwa kwa dhamana, huku akisema haoni sababu mahsusi za kushikiliwa kwao.
Juzi mchana, Mbowe na wafuasi 12 walikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Songwe kwa madai ya kufanya mkutano wa kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika eneo ambalo hawakupangiwa. Kwa kufanya hivyo, ilielezwa kuwa ni kinyume cha ratiba za wasimamizi wa uchaguzi.
Aidha, Mbowe alithibitisha kwamba Mdude Nyagali, mfuasi mwandamizi na mwanaharakati mwenye ushawishi mkubwa katika chama hicho, anaendelea kushikiliwa na jeshi hilo.
Akizungumza baada ya kuachiwa, Mbowe alisema licha ya kushikiliwa kwa muda, polisi hawajawapa sababu mahsusi za kuwakamata na badala yake wamekuwa wakisingizia mambo aliyoita yasiyo na mashiko.
“Lakini hatimaye usiku huu baada ya kudai kwa nguvu sana wametuachia na wanasema kosa letu ni kuharibu ratiba ya mikutano ya kampeni. Sasa tumeharibu vipi? Sisi hatujui.
"Tumegoma kutoa maelezo yoyote na tuliwaambia kwamba tutakuwa tayari kutoa maelezo hayo kama watatuhakishia kuwa watatufikisha mahakamani,” alisema.
Mbowe amelishutumu Jeshi la Polisi mkoani Songwe kwamba limemkamata kama mkakati wa makusudi wa kuvuruga mikutano yake ya kampeni iliyopangwa katika majimbo ya Mbozi, Vwawa na Tunduma.
KAULI YA SUGU
Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara Kyela mkoani Mbeya, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu, alisema kukamatwa kwao kunatokana na hofu ya Chama Cha Mapinduzi CCM kuondolewa madarakani.
Sugu alisema CCM haikubaliki na Watanzania ndiyo maana inaogopa kuondolewa madarakani, hivyo imeamua kutumia vyombo vya dola kuwakamata viongozi wa upinzani, hususan wa CHADEMA.
“Hivi sasa kazi tuliyo nayo ni moja tu ya kuiondoa CCM madarakani kwani imechoka na haikubaliki ndiyo maana inatumia mabavu kutisha wananchi na kutumia vyombo vya dola kuwakamata viongozi wa CHADEMA.
“Ukweli ni kama walivyofanya jana (juzi) kule Songwe walipotukamata mimi na Mwenyekiti Mbowe pamoja na viongozi wengine na ‘staff’ (maofisa) wa Mwenyekiti. Hawana hoja ya maana, hivyo wameamua kutumia mabavu kuendelea kubaki madarakani,” alisema Sugu .
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Augustine Senga, alisema jana wanaendelea kumshikilia Nyagali kwa sababu ya kuwa na mashtaka mengine, lakini akitekeleza masharti ya dhamana watamwachia.
Alisema viongozi na wafuasi wa chama hicho walioachiwa watatakiwa kuripoti tena polisi Novemba 28, mwaka huu, kama masharti ya dhamana yanavyoelekeza.
Viongozi wengine walioachiwa ni Mwenyekiti wa chama hicho, Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu, Mbunge mstaafu wa Mbozi, Paschal Haonga, na Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo mkoani Songwe, Elia Zambi.
Wafuasi wa chama hicho waliokamatwa juzi ni Adamu Kasekwa (35), Halfan Mbire (37) na Mohammed Ling'wanya (walinzi).
Wengine ni waandishi wa habari wawili, Apolinary Margwe na Keneth Ndabila pamoja na Paul Joseph (ofisa wa chama) na Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mbozi, Michael Msongole.
Juzi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, liliwakamata viongozi na wafuasi 12 akiwamo Mbowe kwa madai ya kufanya mkutano wa kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika eneo ambalo hawakupangiwa jambo ambalo ni kinyume cha sheria na ratiba za wasimamizi wa uchaguzi.
from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/onyrQL1
via IFTTT