KUNA kitu kinaendelea chini kwa chini pale Yanga na lolote linaweza kutokea kwenye dirisha dogo la usajili linalofunguliwa Desemba 15.
Yanga imepania kufanya mabadiliko kadhaa kwenye safu yake ya uchezaji na mmoja kati ya watakaoingia kuwa mbadala wa Khalid Aucho huenda akawa sapraizi kwa wengi.
Yanga inaendelea na mazungumzo na Singida Black Stars kuangalia uwezekano wa kumpata kwa mkopo, kiungo mkabaji, Kelvin Nashon kama mbadala mpya wa Aucho. Msimu huu hajakiwasha sana akiwa na Singida kutokana na majeruhi lakini akiwa na Geita Gold akicheza sambamba na Yusuf Kagoma aliyehamia Simba alikiwasha sana na ndipo jina lake lilipoanza kuwaka.
Nashon ni kati ya viungo wakabaji wazawa wanaofanya vizuri katika Ligi Kuu Bara ambapo msimu huu amekuwa akiitumikia Singida Fountain Gate aliyojiunga nayo kipindi cha usajili wa dirisha dogo msimu wa 2022/23 akitokea Geita Gold kwa mkataba wa miaka miwili.
Amebakiza miezi sita kumaliza muda wake ambapo viongozi wa usajili wa Yanga wanadhani ndiye mbadala sahihi wa Aucho kwani itawasaidia kupunguza presha kwenye usajili wa wachezaji wa kigeni kipindi hiki cha kumaliza msimu. Ingawa hajapata muda mrefu wa kucheza Yanga wanaamini uzoefu wake pale kati anacheza.
Kiungo huyo amekosa namba kikosi cha kwanza cha Singida mbele ya Emmanuel Keyekeh aliyetokea FC Samartex ya kwao Ghana, Josaphat Arthur Bada aliyetokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast, huku mwingine akiwa ni Mohamed Damaro aliyetoka Hafia FC ya Guinea.
Nyota hao kiujumla wamechangia mabao 10 kati ya 16 yaliyofungwa na Singida msimu huu, ambapo Keyekeh amefunga mawili na kuchangia pia mawili, huku Josaphat akitupia kambani mawili na kuasisti matatu, wakati Damaro amefunga bao moja tu.
Taarifa za uhakika zilizoifikia Mwanaspoti zinabainisha kuwa Yanga wamewasiliana na viongozi wa Singida BS kwa ajili ya kuitaka huduma ya Nashon kwa mkopo wa miezi sita na asilimia kubwa mambo yanaenda vizuri na huenda dili hilo likamalizika kabla ya dirisha dogo kufunguliwa.
Habari za uhakika zinabainisha kwamba sababu Yanga kumuhitaji zaidi Nashon ni kwa ajili ya kuwa mbadala wa kiungo wao Khalid Aucho raia wa Uganda kwani wakimkosa mchezaji huyo wanakuwa na changamoto ya mbadala wake.
“Kati ya sehemu zakuboresha kwa ajili ya msimu ujao ipo nafasi ya kiungo mkabaji ndiyo maana wameangukia kwa Nashon ambaye maombi yao ni miezi sita kupisha dirisha kubwa mwakani,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza.
“Ukiangalia ndani ya Yanga ukimuondoa Aucho, kuna Jonas Mkude na Salum Abubakar 'Sure Boy', Aziz Andambwile na Duke Abuya wanaocheza nafasi moja, hivyo benchi la ufundi limeona kuna haja ya kitu kifanyike kulingana na matakwa yao.”
Nashon msimu uliopita kabla ya kujiunga na Singida Black Stars akiwa Geita Gold alitajwa kujiunga na Simba lakini mambo yalikwenda tofauti kutokana na dau alilopewa na waajiri wake wa sasa dirisha hili kwake ni rahisi kuchomoka kutokana na ukame wa nafasi ndani ya kikosi hicho.
Licha ya kukosa nafasi Singida Black Stars kiufundi Yanga wanaamini ana nafasi kubwa ya kucheza ndani ya kikosi chao kutokana na eneo hilo kutokuwa na ushindani mkubwa kwani Aucho ndiye mwenye uhakika wa namba kikosi cha kwanza na anatajwa kubakiza miezi sita kwenye mkataba wake.
Mwanaspoti lilimtafuta kiungo huyo ili aweze kuzungumzia mchakato huo alisema "Siwezi kuzungumzia suala hilo kwasasa mimi bado ni mchezaji halali wa Singida Black Stars kwa mujibu wa mkataba.''
from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/mJvs0EA
via IFTTT