Rais Samia Afanya Uteuzi na Mabadiliko Baraza la Mawaziri



BAADA ya miezi minne, Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo tena katika Baraza lake la Mawaziri:

Innocent Bashungwa na Dk. Damas Ndumbaro ni miongoni mwa mawaziri wanaoongoza kusimamia wizara nyingi tangu Rais Samia aingie madarakani Machi 19, 2021.

Miongoni mwa wizara alizohudumu Bashungwa ni za Ujenzi, Biashara na Viwanda na Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Jerry Silaa, aliyewahi kuhudumu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na sasa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naye ameguswa katika mabadiliko hayo.

Sekta ya Habari ambayo ilikuwa sehemu ya wizara anayosimamia Silaa, imerejeshwa ilikokuwa wakati wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete -- Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mawaziri wengine walioguswa ni Dk. Ashatu Kijaji, ambaye amewahi kuhudumia Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha na Mipango, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Mwingine ni Dk. Damas Ndumbalo, ambaye alianzia Wizara ya Katiba na Sheria, kisha Maliasili na Utalii; Michezo, Sanaa na Utamaduni na sasa amerejeshwa tena Wizara ya Katiba na Sheria.

Katika uteuzi huo, pia kuna sura mpya hasa katika nafasi ya ubalozi, wamo waliotolewa kwenye majukumu yao ya awali na kutakiwa kupangiwa kazi nyingine.


Rais Samia pia ameunda Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, sekta hiyo ikiondolewa kutoka iliyokuwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Katika hilo, Rais Samia amemteua Prof. Palamagamba Kabudi, kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamad Yusuph Masauni ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Prof. Kabudi alirejeshwa kwenye uwaziri Agosti 14 mwaka huu na kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.


Wengine walioteuliwa ni Abdallah Ulega anayekuwa Waziri wa Ujenzi, akichukua nafasi ya Bashungwa aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Gerson Msigwa, amerudishwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, lakini akiongezwa jukumu lingine la kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali.

Dk. James Kilabuko, ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk. Stephen Nindi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayeshughulikia masuala ya ushirika na umwagiliaji wakati Dk. Suleiman Serera amehamishwa kutoka Wizara ya Kilimo kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda Biashara.

Prof. Mohamed Janabi ameteuliwa kuwa Mshauri wa Rais - Masuala ya Afya na Tiba ambaye pamoja na nafasi hiyo ataendelea kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Balozi Dk. John Stephen Simbachawene atapangiwa kituo cha kazi, Anderson Mutatembwa, Mobhare Matinyi, Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad, Kamishna wa Polisi CP Suzan Kaganda pamoja na aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba wameteuliwa kuwa mabalozi na watapangiwa vituo vya kazi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu jana, uapisho wa viongozi walioteuliwa, utafanyika Ikulu ndogo Zanzibar kesho Desemba 10.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TANZANIA), Edwin Soko, alisema wanabariki uteuzi katika Wizara ya Habari na kwamba lengo kuu ambalo wao wanataka kama wanatasnia ni kuona matokeo na Sekta ya Habari isimezwe inapowekwa katika wizara fulani.

"Cha msingi ni kuona matokeo yawe vipi. Je, inasimamia uhuru wa habari, tuna sheria rafiki, ikizungumza au wanatasnia wakizungumza inaguswa, ina matokeo yapi kila eneo?" alisema Soko.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, alisema awali wadau waliomba Sekta ya Habari ihamishwe kutoka Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo ndipo ikapelekwa Mawasiliano kwa kuwa ilimezwa na mawaziri wengi kuipa kisogo.

"Rais imempendeza kuirejesha kule pa awali, tunaamini waliopewa dhamana hawataiweka kando Sekta ya Habari kama ilivyokuwa awali. Faraja tuliyoipata ni kwamba viongozi wakuu wote walioteuliwa ni wanahabari," alisema.

S


from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/VQBGUTw
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post