Tathmini ya mitaani pamoja na mitandaoni inaonyesha mashabiki wa Yanga wamekosa imani kutokana na matokeo ya siku za hivi karibuni kwenye michuano mbalimbali.
Lakini kocha wao, Sead Ramovic ameibuka na mkakati ambao anaamini utasaidia kurejesha kasi ya uwajibikaji kikosini hapo hususani kwenye mechi za kimataifa ambako piga ua lazima Yanga ipate pointi tatu katika mechi ijayo dhidi ya TP Mazembe ugenini kama bado inahitaji kucheza robo ya Ligi ya Mabingwa.
Ufanisi wa baadhi ya mastaa ambao hakuwataja majina umemtibua Ramovic akashusha mkwara mzito, kuanzia sasa hawaangalii historia ya mchezaji bali kile anachokifanya kwa wakati uliopo kinavyochangia matokeo chanya.
Ramovic aliliambia Mwanaspoti anachekecha kiwango cha wachezaji wake kwenye mechi wanazocheza na mazoezini na anajua aina gani ya maboresho anayoyataka kwa wachezaji wake na ripoti ya ufanisi wao itamsaidia kujua anamhitaji nani kuendelea naye katika madirisha ya usajili yanayokuja.
“Tunafuatilia kwa karibu mchango wa kila mchezaji aliyepo hapa, hatutabaki na mchezaji kwa kutumia historia yake ya nyuma, tutatumia ripoti hizi kufanya maboresho ya kikosi chetu,” alisema kocha huyo huku ikielezwa amewaambia viongozi anataka wachezaji wasiopungua sita kwenye dirisha dogo linaloanza Jumapili ijayo.
Mwananchi linajua anataka kipa ambaye haachani mbali na Djigui Diarra, beki wa kushoto, kati, kiungo na mshambuliaji anayeliona goli.
“Nilisema awali tuna kikosi kizuri lakini uzuri wa kila mchezaji lazima uonekane, sasa kwenye nyakati hizi ambazo tunakosa matokeo mazuri, hii ni timu ambayo inahitaji ushindi karibu kila mchezo,” aliongeza Ramovic.
Ramovic amechekelea kuimarika kwa wachezaji wake wanne na watatu kati ya hao hawakuwahi kabisa kucheza tangu atue klabuni hapo ambao ni kiungo Khalid Aucho, beki Chadrack Boka, mshambuliaji Clement Mzize huku nahodha wake msaidizi Dickson Job naye akirejea.
Mzize na Aucho waliumia misuli wakiwa timu za taifa wakati Boka akianza kuumia kwenye mchezo dhidi ya Singida Black Stars kisha kutonesha kwenye mechi ya Azam FC huku Job akiumia kwenye mechi dhidi ya Namungo kifundo cha mguu.
“Tangu nimefika hawa wachezaji (Boka, Aucho na Mzize) hawakuwa sawa nadhani kwa maendeleo yao tuna nafasi kubwa kuwaona wakicheza mechi ijayo, itakuwa ni kitu kizuri kuona nguvu yao inarudi kuungana na wenzao, pia Job anaweza kuwa tayari pia,” aliongeza kocha huyo.
Yanga haijashinda mechi yoyote wala kufunga bao lolote kwenye kundi lao ikipoteza mechi zote mbili za kwanza ikijiandaa kukutana na Mazembe ambayo ipo juu yao kidogo nafasi ya tatu ikipoteza mechi moja na kutoa sare moja.
“Tuna timu nzuri bahati mbaya hapa ni kwamba hizi mechi mbili za ligi ya mabingwa tumekosa matokeo mazuri, kila mmoja inamuumiza lakini bado tunatakiwa kuamka kwa haraka na kubadilisha mambo,” alisema Ramovic.
Yanga itakutana na Mazembe Desemba 14 Uwanja wa Mazembe jijini Lubumbashi na mabingwa hao wa soka wa Tanzania watahitaji ushindi kufufua hesabu za kusonga mbele na endapo itapoteza mechi hiyo itajiweka kwenye wakati mgumu kwenye kundi lao A linaloongozwa na Al Hilal wenye pointi sita wakifuatiwa na MC Alger wenye pointi nne.
from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/1G76vYN
via IFTTT