HATIMAYE Msajili wa Vyama Afunguka: Mahakama Pekee Ndio Inaweza Kuzuia Uchaguzi Tanzania

HATIMAYE Msajili wa Vyama Afunguka: Mahakama Pekee Ndio Inaweza Kuzuia Uchaguzi Tanzania

Msajili wa vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Francis Mutungi amesema kauli ya ‘No reform, no Election’ bado haijavunja sheria ya vyama vya siasa, huku akisisitiza kuwa uchaguzi mkuu 2025 uko palepale.

Jaji, Mutungi amesema wakati anazungumza na waandishi wa habari baada ya kushiriki warsha ya wadau wa kujadili namna ya kuzuia na kupambana na rushwa katika uchaguzi mkuu 2025.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi wa ndani, CHADEMA wamekuwa wakieleza kuwa, bila mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi hakutakuwa na uchaguzi mkuu mwaka 2025 na kwamba watauzuia kwa kuandamana nchi nzima kauli ambayo inapingwa na vyama vingine vya siasa ikiwemo CCM.

Msajili huyo amesema hakuna anayeweza kuzuia uchaguzi wa mwaka huu, kwakuwa kinachosemwa ni matamshi ya wanasiasa majukwaani ambayo kila chama kinaweza kuwa na maana yake.

“Hakuna awezaye kuzuia uchaguzi kwa kutamka tu kwenye majukwaa, CHADEMA hawajavunja sheria na nilipokutana nao hivi karibuni walisema hawatakuwa tayari kuvunja sheria za uchaguzi,” amesema Jaji Mutungi.

Aidha, amesema chombo kinachoweza kuzuia uchaguzi ni mahakama na hadi sasa hakuna aliyekwenda huko isipokuwa kinachoendelea ni matamshi ya midomoni mwa wanasiasa.

Amesema hajasikia kuwa CHADEMA wamekwenda mahakamani kupinga uchaguzi licha ya kuwa wanao wanasheria wanaojua utaratibu mzima wa nini kifanyike hivyo kinachoonekana ni kama wanafanya propaganda za kisiasa ambazo haziwezi kuwatia hatiani isipokuwa kama kutakuwa na maneno mengine ndani ya kauli zao.

“Mimi nitatafuta muda wa kuwaiteni kuzungumza kirefu zaidi kuhusu mambo haya, lakini kama ulivyosema mimi ndiye baba wa vyama vya siasa ni kweli, na kila chama kina haki ya kusikilizwa lakini siyo kuvunja sheria, sisi hatutegemei kama wanaweza kuvunja sheria,” amesema.



from UDAKU SPECIAL https://ift.tt/5vHSrz0
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post